BAWA MAANA YAKE NINI?
HISTORIA FUPI YA BAWA
Neno BAWA linatokana na msemo wa Kiingereza “Birds of a feather flock together”. Maana yake katika Kiswahili ni kwamba “Ndege wa BAWA moja huruka pamoja / hukusanyika pamoja / hutembea pamoja”. Kwa kihaya: “Obunyonyi bw’oruganda rumoi buharara hamoi”.
CHIMBUKO LA UMOJA WA BAWA
BAWA ilianzishwa na mafrateri wa Bukoba waliokuwa wakisomea Seminari Kuu ya Katigondo, Uganda. Lengo lao lilikuwa, kama lilivyo sasa, kuimarisha umoja na mshikamano kati ya mafrateri wenyewe, waweze kupaa pamoja kama ndege wa BAWA moja hadi kufikia wito wao, yaani UPADRE. Mwaka 1964, Seminari Kuu ya Ntungamo ilifunguliwa kwa ajili ya masomo ya Falsafa na Teolojia. Hivyo Bukoba haikupeleka tena mafrateri Katigondo; na polepole wazo la BAWA likaanza kusahaulika. Mwaka 1967, Seminari kuu za Ntungamo na Kibosho (Moshi) zilianza kufundisha Falsafa tu, zikipokea wanafunzi kutoka Tanzania nzima; na Kipalapala kikawa Chuo cha Teolojia kwa ajili ya mafrateri kutoka Tanzania nzima. Mafrateri wa Bukoba wa Kipalapala, wakitambua umuhimu wa mshikamano kuelekea lengo lao moja walifufua tena umoja, wakihamasishana kwa msemo uleule kwamba, “Ndege wa BAWA moja huruka pamoja”. Walizoea kuitana “mafrateri wa bawa moja” na hatimaye neno “BAWA” likawa jina halisi la umoja wao.
Siku zilivyosogea, neno BAWA lilizidi kupata umaarufu, hatimaye likawa jina la umoja wa mafrateri wa Jimbo la Bukoba katika Seminari kuu zote nne, yaani Kipalapala, Segerea, Ntungamo na Kibosho. Mapadre wote wa Jimbo la Bukoba waliosomea katika Seminari hizi walibaki na kumbukumbu nzuri juu ya umoja huu, wakaendelea kujitambua kama wanaBAWA halisi. Ni kwa namna hii BAWA ilipata kuwa UMOJA WA MAFRATERI NA MAPADRE WA JIMBO LA BUKOBA, na ndivyo ilivyo hadi sasa katika ujumla wake.
UHAI WA BAWA
Uhai wa BAWA upo katika utendaji wa kazi zake muhimu ambazo ni kusaidiana katika kuelekea wito wa upadre pamoja na katika kuuishi huo upadre baada ya kufika. Katika kupaa pamoja, ndege wote husaidiwa kubaki katika kundi na kuepusha kutawanyika kwa ndege hao ambako huweza kusababisha baadhi yao kushambuliwa na wanyama wakali.
WanaBAWA wamekuwa wakisaidiana kiroho, kiushauri, kielimu, kiuchumi na katika mambo yote ambayo husaidia kumjenga mseminarista au padre kiutu na kiwito. Umoja wa BAWA umekuwa msaada mkubwa kwa mafrateri na waseminari; wale walio katika malezi na wale ambao tayari wanafanya kazi katika shamba la Bwana kama mapadre na hata maaskofu. BAWA umekuwa kama punje ya haradali aliyotwaa mtu akaitupa katika shamba lake; ikamea, ikawa mti; ndege wa angani wakakaa katika matawi yake.(Lk. 13:19)
Ni jukumu la wanaBAWA wote kuuendeleza umoja huu na kuufanya uwe wa msaada zaidi hasa katika changamoto mbalimbali zinazojitokeza katika maisha yao. Mafrateri wa BAWA katika Seminari kuu wameendelea kuhuisha na kuimarisha umoja huu kwa njia ya mikutano na chaguzi za viongozi wanaokuwa mbele katika kushughulikia mambo mbalimbali yanayowagusa kwa ujumla kama mafrateri wa Jimbo la Bukoba.
Umoja wa BAWA hutegemezwa na michango ya kila mwaka, kutoka kwa kila frateri kama wajibu, na michango ya hiari kutoka kwa mapadre wanajimbo. Michango hii husaidia kutatua matatizo hasa ya kiuchumi kati ya wanaBAWA. Pia michango hii husaidia katika kufanikisha uchapishaji wa gazeti hili la BAWA ambalo kawaida hutolewa kila mwaka.
GAZETI LA BAWA
Hili ni Gazeti linalochapishwa na mafrateri wa jimbo la Bukoba.
Madhumuni ya Gazeti:
Gazeti hili huchapisha na kuweka kama hazina mambo mbalimbali yanayowafaa au yatakayowafaa wanaBAWA wawapo seminarini na hapo baadaye huko jimboni katika kutekeleza kazi zao. Hivyo gazeti hili huchapisha mambo ya kiuchungaji, jadi na kiutamaduni hasa yahusuyo dini pamoja na utafiti mbalimbali. Kwa ufupi gazeti hili ni kama uwanja wa kubadilishana mawazo kati ya Mapadre, Waseminarista, Watawa, waumini na watu wote wenye mapenzi mema wa jimbo la Bukoba na hata nje ya Jimbo la Bukoba.
Makala:
Gazeti huchapisha makala mbalimbali. Makala kawaida huandikwa kwa lugha ya Kiswahili au kihaya. Makala za kiingereza zaweza kuandikwa japo itakuwa vizuri zaidi zikitafsiriwa kwa Kiswahili au kihaya ili kuwasaidia wasomaji wengi, ambao si wote wanafahamu kiingereza vizuri, waweze kuelewa. Mwandishi wa makala aweza kuwa Padre, Mseminarista au hata mtawa.
Mada zinazochapishwa na gazeti hili yaweza kuwa juu ya jambo lolote la kitafiti, kihistoria au la utunzi na hasa katika mambo yafuatayo:
Ø Mtu (Binadamu): tangu kuzaliwa hadi kufa (taratibu mbalimbali, ibada, miiko n.k.
Ø Majina mbalimbali: aina za majina na maana yake.
Ø Uchumba na ndoa:(a very wide topic for research)
Ø Kifo: maana, chanzo, mazishi, misiba, matanga n.k.
Ø Urafiki na mahusiano mbalimbali(emikago/okunywana).
Ø Historia ya dini Bukoba: dini za jadi na ukristu, vina uhusiano? Ipi ina uzito zaidi n.k.
Ø Embandwa: ni nini? Hufanya nini? Hupatikanaje? Bado wapo?
Ø Hesabu: za hela, saa (wakati) miezi, miaka n.k. kiutamaduni.
Ø Aina: za migomba, vyakula, n.k.
Ø Teknolojia mbalimbali: kama uhunzi, umeme, kompyuta n.k.
Ø Sadaka mbalimbali: za kiutamaduni na za Kikristu
Ø Maadili mema: kulingana na mila njema na mafundisho ya Kanisa.
Ø Pia makala nyingine zinazofaa zinakaribishwa.
Makala hutumwa kwa Mhariri Mkuu au mmojawapo wa wana bodi ya wahariri kwa kutumia anwani zilizoainishwa kwenye jalada la gazeti hili.
Uhariri:
Gazeti hili linayo bodi ya wahariri inayoundwa na Mhariri Mkuu ambaye ndiye mkuu wa Bodi hiyo akisaidiwa na Mhariri Mkuu msaidizi pamoja na wahariri wengine kama walivyoorodheshwa uk. 4. Hawa huchaguliwa na mafrateri wa BAWA na hutumikia kwa muda wa Mwaka mmoja.
Bodi ya wahariri huchunguza makala, kuzirekebisha, kuamua makala ngapi zichapishwe katika toleo la BAWA na pia kuamua BAWA itolewe mara ngapi katika utumishi wake kulingana na uwezo wake kifedha na kimakala.
Usambazaji:
Baada ya kuchapishwa gazeti husambazwa na mafrateri wa BAWA ambapo wafadhili, mafrateri wote na wengine wote waliotuma makala zao hupata nakala mojamoja.
Gharama za Uchapishaji:
Gharama za kuchapa gazeti hili hutokana na michango ya kila mwaka, kutoka kwa kila frateri kama wajibu, na michango ya hiari kutoka kwa mapadre wanajimbo ambao ndio wafadhili wetu wakuu.
Hata hivyo michango hii bado ni kidogo kuhakikisha uchapishaji wa gazeti hili walau mara moja kila mwaka. Ndiyo maana wakati mwingine miaka mingine hupita bila gazeti hili kuchapwa. Hivyo tunaendelea kuwaalika wanaBAWA pamoja na wengine wenye mapenzi mema ndani na nje ya jimbo watuunge mkono katika kufadhili gazeti hili ili liweze kuendelea kuzaa matunda kama lilivyofanya siku zote.